News
DONDOO MUHIMU KUTOKA KWENYE UTAFITI WA VIASHIRIA VYA VVU WA MWAKA 2022 – 2023 (THIS 2022-2023)
Tanzania hufanya utafiti kila baada ya miaka mitano ili kuangazia mwenendo na hali ya maambukizi ya VVU nchini. Utafiti wa hivi karibuni uliofanyika mwaka 2022 – 2023 uliangazia mwenendo wa ushamiri wa VVU kitaifa na kimkoa, kiwango cha maambukizi mapya kwa ngazi ya taifa na utumiaji wa huduma za kinga. Aidha, utafiti huu uliangalia pia hatua ambazo Tanzania imefikia katika malengo ya 95-95-95.
Kiwango cha ushamiri wa VVU
Kutokana na utafiti huo (Tanzania HIV Impact Survey - THIS, 2022-2023), kiwango cha ushamiri wa VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea, kimepungua kutoka asilimia 4.9 kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2016- 2017 hadi kufikia kiwango cha asilimia 4.4. Utafiti umeendelea kubainisha kwamba kiwango cha ushamiri wa VVU ni kikubwa miongoni mwa Wanawake kwa asilimia 5.6 ukilinganisha na Wanaume wenye kiwango cha asilimia 3.0.
Kwa upande wa Tanzania bara, mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya ina ushamiri wa VVU zaidi ya asilimia 9 (Njombe asilimia 12.7, Iringa asilimia 11.1, Mbeya asilimia 9.6) . Mikoa ya Kigoma, Manyara na Lindi imetajwa kuwa na kiwango kidogo cha ushamiri wa VVU (asilima 1.7 Kigoma, asilimia 1.8 Manyara na maambukizi ya VVU.
Maambukizi Mapya ya VVU
Maambukizi mapya yamebainika kuwa ni takribani watu 60,000 kwa mwaka huku ikibainishwa kwamba Vijana miaka 15-24 wanachangia zaidi ya theruthi moja (asilimia 33) ya maambukizi yote. Miongoni mwa vijana, vijana wa kike wanachangia zaidi ya robo tatu (asilimia 78) ya maambukizi mapya yanayotokea miongoni mwa vijana.
Ufubavu wa VVU
Utafiti huo umeangazia pia ufubavu wa VVU kwa WAVIU ambapo imebainika kwamba Mkoa wa Tanga umefanya vizuri kwa kuwa na kiwango cha ufubavu kwa asilimia 93.5 na Mkoa wa Tabora umebainika kuwa na kiwango cha chini cha ufubavu wa VVU kwa asilimia 65.8.
Mafanikio ya malengo ya 95 – 95 – 95
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS), liliweka malengo ya 95 – 95 – 95 yaliyoazimia kuhakikisha kwamba asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) wanapima na kujua hali zao za maambukizi, asilimia 95 ya watu wanaogundulika kwamba wanaishi na maambukizi ya VVU wanaanza kutumia dawa za kufubaza VVU (ARV) na watu wanaotumia dawa wanafubaza VVU kwa asilimia 95. Utafiti umebaini kwamba, Tanzania imefikia mafanikio yafuatayo katika malengo hayo; asilimia 82.7 ya watu wanaoishi na VVU wamepima na kujua hali zao za maambukizi, asilimia 97.9 ya WAVIU wameanza kutumia dawa za kufubaza Virusi Vya UKIMWI (ARV) miilini mwao, na WAVIU wanaotumia dawa za ARV wamefubaza VVU kwa asilimia 94.3.
Wananchi wanaendelea kusisitizwa kwamba UKIMWI bado upo hivyo ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari za dhati kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU ikiwa ni pamoja na kupima ili kujua hali zetu za maambukizi ya VVU, kutumia kinga dhidi ya maambukizi ya VVU kama vile kondom na kinga nyinginezo, na kwa wale waliogundulika kwamba wanaishi na maambukizi ya VVU watumie kwa usahihi dawa za kufubaza VVU (ARV) pamoja na ushauri wanaopewa nawatoa huduma za afya.