Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania
The Prime Minister's Office

Tanzania Commission for AIDS

Tanzania Commission for AIDS

News

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA UKIMWI YAFANYA ZIARA - NJOMBE


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI Mhe. Elibarik Kingu amepongeza mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kuhakikisha Watu wanaoishi na VVU (WAVIU) wanaweza kushiriki shughuli za maendeleo na kujipatia kipato

Mhe. Kingu ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea kikundi cha WAVIU cha Jipime Labor Construction kilichopo Kijiji cha Mundindi kata ya Mundindi, wilaya ya Ludewa mkoani Njombe. Pamoja na hayo Mhe. Kingu amewapongeza wanakikundi kwa kutoogopa unyanyapaa na kuungana kwa pamoja kufanya kazi zinazowainua kiuchumi.

Aidha, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga ametoa shukurani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa Ludewa na kuwaletea miradi mbalimbali ikiwemo inayowalenga WAVIU. Mhe. Nderiananga amewasisitiza WAVIU kuendelea kujitokeza na kujiunga kwenye vikundi ili waweze kunufaika zaidi na kukuza vipato vyao.

Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi cha JIPIME Ndg. Marianus Mkinga ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwakumbuka wananchi wa Ludewa wasioishi na wanaoishi na maambukizi ya VVU kwa kuwaletea miradi inayolenga kuwainua kiuchumi.