News
MENEJIMENTI YA TACAIDS YATEMBELEA BANDA LA OFISI YA WAZIRI MKUU - MAONESHO YA NANENANE DODOMA
SERIKALI YATENGA BIL. 277 KUGHARAMIA HUDUMA ZA VVU na UKIMWI
Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI nchini ambapo Kupitia Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI
imepanga kutoa zaidi ya Bilioni 277 kwa mwaka kugharamia huduma za VVU na UKIMWI. Hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa wafadhili katika kugharamia afua za VVU na UKIMWI hapa nchini.
Akiongea mara baada ya kutembelea Banda la Maonesho ya Nane nane la Ofisi ya Waziri Mkuu leo tarehe 6 Agosti, 2025 jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI-TACAIDS, Dkt. Samwel Sumba, amebainisha kuwa
Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuimarisha upatikanaji wa fedha za ndani ili kugharamia mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini.
“Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI ikiwa ni pamoja na huduma za kinga, matibabu kwa WAVIU na matunzo na kuhakikisha Dawa za Kufubaza Virusi Vya UKIMWI (ARV) zipo za kutosha wakati wote. Takribani 90% ya WAVIU wote nchini wanapata huduma za matibau ya ARV na matunzo”
Dkt.Sumba amesisitiza kuwa zaidi ya 91% ya watu wote wanaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU wanaunganishwa katika huduma za matibabu ya ARV na matunzo katika vituo vya kutolea huduma vilivyopo nchini.
Amesisitiza kupitia maonesho hayo TACAIDS inatoa elimu kwa wananchi kuhusu VVU na UKIMWI ili kupunguza unyanyapaa ambao ni kikwazo kikubwa katika mwitikio wa VVU na UKIMWI. Aidha, ameongeza kuwa Unyanyapaa umepungua toka 28% mwaka 2013 hadi kufikia 5% mwaka 2024 ambapo lengo ni kutokomeza unyanyaa ifikapo mwaka 2026.
“Tuendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi, Tujitokeze kupima kwa hiari ili kujua hali zetu (upimaji wa VVU ni bure) na Kwa ambao tuna maambukizi basi tuhakikishe tunatumia ARV na kuhakikisha tunakuwa wafuasi wa dawa bila kutetereka”
#Tusonge na Samia kutokomeza UKIMWI