Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania
The Prime Minister's Office

Tanzania Commission for AIDS

Tanzania Commission for AIDS

News

VIONGOZI NA WATENDAJI WA TACAIDS WAJENGEWA UWEZO JUU YA MAADILI NA UWAJIBIKAJI


Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na Mameneja wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) wamepatiwa mafunzo juu ya masuala muhimu ya uongozi, maadili na uwajibikaji katika utumishi wa umma ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi, kutoa huduma bora na kufikia malengo yanayowekwa. Mafunzo hayo ya siku tatu yanaendelea jijini Dodoma kupitia wawezeshaji kutoka chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Mkoani Singida.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt Catherine Joachim alisema kwamba Tanzania inajivunia mafanikio kadhaa katika mwitikio wa UKIMWI ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 4.9 mwaka 2016/17 hadi asilimia 4.4 mwaka 2022/23, kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na UKIMWI, kupungua kwa unyanyapaa na ubaguzi kwa Watu wanaoishi na VVU (WAVIU) pamoja na kupiga hatua kubwa katika kuyafikia malengo ya 95 – 95 – 95. Katika mafanikio hayo mchango wa watumishi na viongozi wa TACAIDS unasehemu kubwa kama waratibu wa afua za VVU na UKIMWI nchini.

“Nawapongeza watumishi wenzangu wa TACAIDS kwakuwa tumekuwa sehemu ya mafanikio ambayo nchi yetu imeyafikia katika mwitikio wa VVU na UKIMWI” Alisema Dkt. Catherine.

Akizungumzia juu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Wakurugenzi, Wakuu wa Sehemu na Mameneja wa TACAIDS, Dkt. Catherine alisisitiza kwamba mafunzo hayo ni muhimu kwa taasisi ili kuboresha utendaji kazi na kufikia malengo ambayo TACAIDS imeyaweka.

“Mafunzo haya yatusaidie sisi kama viongozi ndani ya taasisi yetu kuimarisha utendaji wa shughuli zetu za uratibu wa mwitikio wa VVU na UKIMWI hapa nchini pamoja na kuweka mikakati endelevu itakayotusaidia kujipima katika utendaji wetu” alisisitiza Dkt. Catherine

Muwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Emmanuel Tandika, alisema ni muhimu viongozi kuwa na maadili na weledi kwa kuwa ndio wabeba maono ya taasisi.

“Kiongozi wa umma ana wajibu wa kuwa muadilifu, kusimamia maadili ya uwajibikaji, kuwa mbunifu na kuonesha njia kwa watu anaowaongoza” aliongeza Dkt. Tandika.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 10 Machi, 2025 na yanatarajiwa kuimarisha utekelezaji wa shughuli za VVU na UKIMWI ili Serikali ifikie malengo yake ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030