Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania
The Prime Minister's Office

Tanzania Commission for AIDS

Tanzania Commission for AIDS

News

Kikao cha Kamati ya Utekelezaji wa Programu za Kamisheni ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania 17/05/2022


KAMATI YA UTELKELEZAJI WA PROGRAMU ZA KAMISHENI YA TACAIDS YAFANYA KIKAO CHA UFUATILIAJI KATIKA MWITIKIO WA UKIMWI.

Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania TACAIDS, imefanya kikao cha Kamati ya utekelezaji wa Programu ya Mwitikio wa UKIMWI nchini.

Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 17Mei,2022 jijini Dodoma kwa kushirikisha Menejimenti ya TACAIDS ambapo mwendeshaji wa kikao hicho ni Kamisheni ya Tume hiyo.

Lengo la Kikao hicho,ni kufanya ufuatiliaji wa shughuli zinazotekelezwa na TACAIDS kuona kama zimetekelezwa kwa malengo yaliyokusudiwa kwenye Sheria ya Tume ya Kuthibiti UKIMWI Tanzania Na. 22 ya mwaka 2001 na marekebisho yake Na. 6 ya mwaka 2015 na kuwafikia walengwa kama ilivyotarajiwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Programu, Sheikh Khamis Mataka, alisema vikao hivyo ni moja ya ufatiliaji wao kama viongozi wa Tume kufahamu kwa kina namna shughuli zinavyotekelezeka kuendana na mipango iliyopangwa na Tume.

“Vikao hivi kwetu ni muhimu sana kwani huwa tunashiriki wakati wa upangaji kabla bajeti haijapelekwa Bungeni na baada ya kurejea huwa kuna utekelezaji ambao hufanywa na wataalamu wetu, kabla ya kukaa kikao kikubwa cha kamisheni tunakaa kwanza na wataalamu wanatupatia utekelezaji wa mipango yao na kuona kama imeendana na makubaliano tuliyoyaweka awali”alisema Sheikh Mataka.

Kikao hiki ni utangulizi wa vikao viwili vya programu vilivyopangwa kufanyika wiki hii kwa lengo la ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya TACAIDS kulingana na utaratibu uliowekwa na Kamisheni ya Tume ambayo imeundwa kwa kumujibu wa sheria iliyounda TACAIDS.

Naye Mratibu wa vikao hivi ambaye pia ni mwanasheria wa TACAIDS Bw. Miraji Mambo amesema kamisheni ya TACAIDS imeundwa kwa mujibu wa sheria na ina wajumbe kumi na moja, ambao ndio wanaongoza TACAIDS kwa kusimamia sekretarieti katika utekelezaji wa majukumu yote ya Tume.

Bw.Miraji amesema kuwa kwa mujibu wa utaratibu kamati hizi zipo mbili;Kamati ya programu,ilikutana leo, ambayo inafuatilia zaidi utendaji wa shughuli za tume na kamati nyingine ya fedha itakutana tarehe 18 Mei,2022 ambayo kazi yake kubwa ni kuangalia kwa kina matumizi sahihi ya fedha za TACAIDS. Aidha, kikao cha 49 cha Kamisheni hiyo kitafanyika tarehe 24 Mei, 2022 kwa ajili ya kujadili pamoja na mambo mengine taarifa kutoka kwenye Kamati ya Utekelezaji wa Programu na Kamati ya Fedha.

Baada ya kumaliza kikao mwenyekiti aliwashukuru Sekretarieti kwa maandalizi mazuri ya taarifa za utekelezaji wa programu na kuagiza utaratibu huo waendelee nao kwa maana kwamba Kamisheni ifanye kazi yake na sekretarieti ifanye kazi yake ili kufikia malengo ya Tume yaliyosukudiwa.