News
KONGAMANO LA VIJANA KUJADILI MASUALA MUHIMU YA UKIMWI
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe iliandaa kongamano lililohusisha takriban wanafunzi 1600 kutoka baadhi ya shule 72 za msingi na sekondari zilizopo mkoani Njombe. Lengo likiwa ni kujadili na kutoa elimu kwa vijana kuhusu mambo muhimu ya VVU na UKIMWI, Afya ya Uzazi pamoja na maadili.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mhe. Zakaria Mwansasu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe alisisitiza kwamba. Ili kuwa na taifa bora lazima vijana wajengewe msingi katika mambo muhimu ikiwemo masuala ya Afya na Maadili. Hivyo, makongamano haya yatasaidia kuwajenga vijana na kuwajengea uwezo wa kulinda afya zao
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt Catherine Joachim alisisitiza kwamba vijana wamekuwa wakipata changamoto nyingi katika kufikia huduma mbalimbali ikiwemo za afya. Dkt Catherine aliendelea kusisitiza kwamba kutokana na takwimu za viashiria vya VVU/UKIMWI za mwaka 2022/2023 imebainika kwamba vijana wanakiwango kikubwa cha maambukizi. Hivyo TACAIDS inatumia majukwaa mbalimbali ikiwemo makongamano ili kutoa elimu kwa vijana